Katika kujadili swali hili tutaanza na
utangulizi kwa kueleza maana ya asili,
maana ya msamiati na baada ya hapo tutaangalia jinsi kigezo cha msamiati
kinavyotumiwa kudai kuwa Kiswahili ni
kiarabu na tutaonesha udhaifu wake na mwisho tutakanusha madai haya kwa
kuonesha kuwa Kiswahili ni kibantu na sio kiarabu.
Mjadala kuhusu asili ya Kiswahili umejadiliwa
na wataalam mbalimbali na wametumia vigezo mbalimbali kuthibitisha madai yao.
Wapo wanaodai kuwa Kiswahili ni kiarabu, wanaoshadidia dai hili, kigezo
kimojawapo wanchokitumia ni kigezo cha msamiati, kwamba lugha ya Kiswahili ina
msamiati mwingi wa kiarabu na kwa hiyo kwa kuwa Kiswahili kina msamiati mwingi
wa kiarabu basi pia Kiswahili ni kiarabu, kwa kweli dai hili halina mashiko.
Kabla hatujaanza kufafanua kwamba kwa nini dai hili halina mashiko ni vema tukaangalia fasili ya dhana muhimu
kama zinavyojitokeza katika swali la mjadala. Dhana hizo ni kama zifuatazo:
‘Istilahi asili,’ kwa mujibu wa Massamba na wenzake (1999)
asili ni jinsi kitu au jambo
lilivyotokea au lilivyoanza. Fasili hii
ni nzuri na inajitosheleza kwa maana kwamba jambo au kitu kinaweza kutokea
kibahati kama ilivyo katika lugha au linaweza kuanzishwa.
Msamiati pia unaelezwa na TUKI (2004) kuwa ni jumla ya
maneno katika lugha. Fasili hii iko wazi kwamba jumla ya maneno yote katika
lugha ndio huunda msamiati wa lugha husika.
Wataalam wanaodai kuwa Kiswahili ni kiarabu
kwa kutumia kigezo cha msamiati, hoja zao ni kama zifuatazo:
Khalid (2005) anasema kuwa neno lenyewe
Kiswahili limetokana na neno la kiarabu sahil katika umoja ambalo wingi
wake ni sawahili likiwa na maana
ya pwani au upwa. Hivyo kutoka na jina la lugha hii ya Kiswahili kuwa na asili
ya neno la kiarabu sahil hivyo hudai kuwa Kiswahili ni kiarabu.
Khalid anaendelea kusema kuwa Kiswahili kina
msamiati mwingi wenye asili ya kiarabu. Hapa ni baadhi ya mifano ya msamiati wa
Kiswahili wenye asili ya kiarabu kama alivyobainisha Khalid:
Maneno yanayoonesha muda.
Asubuhi dakika
Wakati alfajiri
Karne alasiri
Magharibi saa
Maneno yanayowakilisha namba.
Nusu robo
Sita saba
Tisa ishirini
Thelathini arubaini
Hamsini sitini
Sabini themanini
Tisini mia
Elfu
Mtandao wa jamiiforum pia wameonesha mifano ya msamiati wa Kiswahili wenye asili
ya kiarabu kama ifuatavyo:
Kiswahili Kiarabu
Dirisha drisha
Karatasi kartasi
Debe dabba
Samaki samak
Mustakabali mustakabal
Madrasa madrasa
Lodh (2000) naye anasema kiasi kikubwa cha
nomino za Kiswahili zimetokana na mizizi ya maneno ya kiarabu. Mifano ya maneno
hayo ni kama yafuatayo:
Hesabu/hisabu mahisabu/hisabati
Harka harakati
Safiri - msafiri
Safari -
msafara
Fikiri - fikara/fikra
Hata hivyo kigezo hiki cha msamiati kina
udhaifu; Massamba (2002) ameonesha udhaifu wa kigezo hiki kuwa ni pamoja na
kwamba:
Hakuna ushahidi wowote wa kitakwimu ambao
unaonesha idadi ya maneno ya kiarabu yaliyopo katika lugha ya Kiswahili
yanayoweza kuhitimisha kuwa Kiswahili ni kiarabu.
Kigezo cha msamiati peke yake hakijitoshelezi
kuelezea kuwa Kiswahili ni kiarabu, walipaswa waangalie vigezo vingine kama
vile kigezo cha kihistoria kwa kuchunguza masimulizi mbalimbali ya kale na
kigezo cha kiisimu; katika kigezo hiki walipaswa kuchunguza fonolojia,
mofolojia , na sintaksia ya Kiswahili kwa kulinganisha na kiarabu na ndipo
wangepata hitimisho sahihi la madai yao.
Vilevile kigezo hiki cha msamiati hakina
mashiko kwa sababu lugha ina tabia ya kuathiriana, lugha huathiriana na lugha
nyingine endapo kutakuwa na mwingiliano baina ya wanajamii lugha hizo. Kwa mfano Kiswahili kimetokea kuathiriana na
kiarabu kutokana na uhusiano uliokuwepo hapo zamani katika biashara kati ya
waarabu na watu wa upwa wa Afrika Mashariki na hii ikapelekea msamiatia wa
kiarabu kuingia katika lugha ya Kiswahili, hivyo kwa hoja hii hatuwezi kusema
Kiswahili ni kiarabu kwa sababu msamiati wa kiarabu unaonekana katika lugha ya
Kiswahili.
Hata hivyo si lugha ya kiarabu tu ambayo
msamiati wake unaonekana katika lugha ya Kiswahili vilevile kunamsamiati wa
lugha zingine za kigeni katika lugha ya Kiswahili kwa mfano, neno lenye asili
ya kireno katika Kiswahili ni kama vile meza,
leso pia yapo maneno yenye asili ya kijerumani kwa mfano schule kwa Kiswahili shule na maneno yenye asli ya kiingereza
ni kama vile mashine, televisheni,
sekondari, redio, kompyuta na maneno mengine yenye asli hiyo. Basi ingekuwa
msamiati wa kigeni kuonekane kwenye lugha fulani huifanya hiyo lugha kuwa na
asili ya lugha ya kigeni basi tungesema pia Kiswahili ni kiingereza kwa sababu tu msamiati mwingi wa kiingereza
unonekana katika Kiswahili.
Pia kigezo hiki kinaonekana kuwa ni dhaifu kwa
sababu hawakufanya utafiti katika nyanja zote za matumizi ya lugha kwa mfano
msamiti unaotumika katika nyanja ya elimu, afya, utamaduni na kadhalika. Kwa
hiyo madai haya yanaonekana kutokuwa na mashiko kwa ufinyu wa utafiti wake.
Kutoka na kigezo hiki cha msamiati kutokuwa na
mashiko kuhitimisha kuwa Kiswahili ni kiarabu, basi hatuna budi kusema kuwa
Kiswahili sio kiarabu bali ni kibantu. Katika kuthibitisha madai haya tutajikita zaidi katika kigezo
cha kiisimu ambacho tunaamini kuwa ni kigezo pekee kinachoweza
kutupatia taarifa sahihi kwani ni kigezo cha kisayansi lakini pia tutaangalia
kwa ufupi vigezo ambavyo vinatoa ushahidi juu ya ubantu wa Kiswahili ambavyo ni
ushahidi wa kihistoria, kiakiolojia na kiethinolojia.
Kigezo hiki cha kiisimu kimetumiwa na wataalam
mbalimbali katika kuonesha ubantu wa Kiswahili Massamba (ameshatajwa) amewataja
wataalam mbalimbali ambao wamehusika na utafiti juu ya ubantu wa Kiswahili,
wataalam hao ni pamoja na Carl Meinhof
katika kitabu chake cha Introduction to
the phonology of the Bantu language, Duke
(1935 – 1945), Malcom Guthrie
(1967), Dereck Nurse na Thomas Spear
(1985). Hawa walijadili ubantu wa Kiswahili kwa kutumia kigezo cha kiisimu,
kihistoria na kiakiolojia.
Kwa kuanza na
kigezo cha kiisimu tutaangalia
vipengele kama vile kufanana kwa msamiati wa msingi, muundo wa kifonolojia,
muundo wa kimofolojia, muundo wa kisintaksia mpangilio wa ngeli za majina.
Mizizi ya msamiati wa msingi wa lugha za
kibantu na Kiswahili hufanana kwa kiasi kikubwa, mifano ifuatayo huweza
kuonesha ukweli huu.
Mfano,
Kiswahili
|
Kikurya
|
Kinyiha
|
Kijita
|
Maji
|
Amanche
|
Aminzi
|
Amanji
|
Jicho
|
Iriso
|
Iryinso
|
Eliso
|
Katika mifano hiyo hapo juu tunaona mifano
hiyo hapo juu tunaona kuwa mizizi maji, manche, minzi, manji inafanana kwa
kiasi kikubwa, kwa hiyo huu ni ushahidi tosha kutuonesha kuwa kuna uhusiano wa
kinasaba kati ya Kiswahili na lugha za kibantu.
Pia mofolojia ya Kiswahili na lugha za kibantu
hufanana kwa kiasi kikubwa, yaani mfumo wa
maumbo ya maneno ya lugha ya Kiswahili na lugha za kibatu hufanana. Kwa mfano,
namna viambishi vinavyopachikwa katika mzizi wa maneno hufuata kanuni ileile
kama inavyotumika katika lugha ya Kiswahili yaani viambishi vinaweza kupachikwa
kabla au baada ya mzizi na uwa na uamilifu bayana. Hebu tuchunguze mifano
ifuatayo:
Kiswahili
|
Kisukuma
|
Kisimbiti
|
Kinyiha
|
A-na-lim-a
|
a-le-lem-a
|
a-ra-rem-a
|
i-nku-lim-a
|
a-na-chek-a
|
A-le-sek-a
|
a-ra-sek-a
|
a-ku-sek-a
|
Kwa kuangalia mifano hii utagundua kwamba
katika kutenganisha viambishi hufuata kanuni moja kwamba mahali kinapokaa
kiambishi kwa mfano cha njeo, ndipo pia hukaa kwa upande wa lugha za kibantu,
kwa mfano –na- na –ra- katika lugha ya kisimbiti. Hivyo tunaweza kusema kuwa
kuna unasaba baina ya lugha hizi.
Vilevile sintaksia ya lugha ya Kiswahili na
lugha za kibantu hufanana kwa karibu sana. Kwa mfano jinsi ya mpangilio wa vipashio na
kuunda sentensi hufanana yaani mpangilio wa maneno hufuata kanuni maalum ambazo
hufanana katika Kiswahili na lugha za kibantu. Katika Kiswahili sentesi ina
kuwa na pande mbili yaani upande wa kiima na upande wa kiarifu, katika upande
wa kiima kipashio chake kikuu ni nomino na katika upande wa kiarifu kipashio
chake kikuu ni kietnzi. Hii inamaana kwamba katika kuunda sentensi ni lazima
nomino ianze na baadaye kitenzi. Hebu tuangalie mifano ifuatayo:
Kiswahili
|
Mama / anakula
N (K) T (A)
|
Kijita
|
Mai / kalya
N(K) T (A)
|
Kihehe
|
Mama/ ilya
N(K) T(A)
|
Kihaya
|
Mama / nalya
N(K) T(A)
|
Katika mifano hii tumeona kwamba muunndo wa
kiima-kiarifu katika lugha za kibantu unafanana sana na ule wa Kiswahili yaani
nomino hukaa upande wwa kiima halikadhalika kitenzi hukaa upande wa kiarifu,
kwa hiyo kwa mifano hii tunaweza kusema kuwa lugha ya Kiswahili ni jamii ya
lugha za kibantu.
Pia mfumo wa sauti (fonolojia) wa lugha za kibantu unafana sana
na ule wa Kiswahili, yaani mpangilio wa sauti katika kuunda silabi, na miundo
ya silabi kwa ujumla hufanana. Kwa mfano katika lugha ya Kiswahili hakuna
muundo wa silabi funge yaani silabi ambayo inaishia na konsonanti, muundo
asilia wa silabi za Kiswahili ni ule unaoishia na irabu vilevile katika lugha
za kibantu hufuata muundo wa silabi wazi, yaani silabi zote huishia na irabu.
Mifano ifuatayo hufafanua zaidi:
Kisawhili
|
Baba
|
K+I+K+I
|
Kikurya
|
Tata
|
K+I+K+I
|
Kiha
|
Data
|
K+I+K+I
|
Kijita
|
Rata
|
K+I+K+I
|
Kipare
|
Vava
|
K+I+K+I
|
Tanbihi: K= konsonanti I= irabu.
Kwa mifano hii tunaona kwamba mifumo ya sauti
katika lugha za kibantu hufanana na ule wa Kiswahili, kwa hiyo tunaweza
kuhitimisha kwa kusema kuwa lugha hizi ni za familia moja.
Pia vilevile mfumo wa ngeli za majina katika
lugha ya Kiswahili hufanana sana na ule wa kibantu hususani katika upachikaji
wa maumbo ya umoja na wingi na maumbo ya upatanisho wa kisarufi. Katika lugha ya Kiswahili viambishi vya
umoja na wingi hupachikwa mwanzoni kabla ya mzizi wa neno, hivyohivyo katika
lugha za kibantu. Kwa mfano:
|
Umoja
|
Wingi
|
Kiswahili
|
m-tu
|
wa-tu
|
Kikurya
|
mo-nto
|
abha-nto
|
Kiha
|
umu-ntu
|
abha-ntu
|
Kikwaya
|
mu-nu
|
abha-nu
|
Mifano hiyo hapo juu inadhihirisha wazi kwamba
vipashio vyote vya umoja na wingi hujitokeza kabla ya mzizi wa neno, hivyo ni
dhahiri lugha hizi zina uhusiano wa nasaba moja.
Vilevile katika upatanisho wa kisarufi
lugha za kibantu na Kiswahili huelekea
kufanana viambishi vya upatanisho wa kisarufi hususani viambisha vya nafsi.
Kwa mfano:
Kiswahili
|
Mtoto a-nalia
|
Kizanaki
|
Umwana a-rarira
|
Kisukuma
|
Ng’wana
a-lelela
|
Kikurya
|
Omona a-rakura
|
Tunaona hapo juu kwamba kiambishi ‘a’ cha upatanisho wa kisarufi hujitokeza
katika lugha zote, hivyo tunashawishika kusema kuwa Kiswahili kina uhusiano
mkubwa na kibantu.
Pamoja na
ushahidi wa kiisimu kutupatia vithibitisho tosha juu ya ubantu wa Kiswahili pia
kuna ushahidi mwingine kama vile ushahidi wa kihistoria, kiakiolojia na
kiethinolojia.
Ushahidi wa
kihistoria huchunguza
masimulizi na vitabu mbalimbali vya kale ambavyo huelezea asili na chimbuko la
wakazi wa upwa wa Afrika Mashariki. Vilevile ugunduzi wa kiakiolojia huonesha kuwa kulikuwa na wakazi
wa asili wa upwa wa Afrika Mashariki ambao walikuwa na utamaduni wao na
maendeleo yao hata kabla ya kuja kwa wageni. Katika ushahidi wa kiethinolojia,
huchunguzwa tarihi mbalimbali zinazojaribu kutoa historia ya watu pwani ya Afrika
Mashariki na lugha yao.
Kwa ujumla vyanzo hivi vyote huonesha kuwa
pwani ya Afrika mashariki ilikuwa na wakazi wake wa asili ambao walikuwa na
lugha yao, utamaduni wao na pia maendeleo yao, vyanzo hivi pia huhitimisha kwa
kusema kuwa lugha ya wakazi hawa ilikuwa ni Kiswahili.
Kwa hiyo, kwa hoja hizi tunaweza kuhitimisha
kwa kusema kuwa, madai ya kusema kwamba msamiati mwingi wa kiarabu katika lugha ya Kiswahili hayana mashiko;
Kwani hakuna ushahidi wa kutosha kusimamia hoja hiyo. Kama ilvyojadiliwa hapo
juu,vigezo vya kiisimu, kihistoria, kiakiolojia na kiethnolojia ndivyo vitoavyo
ushahidi wa kina na kutoa hoja za mashiko kuthibitisha kuwa Kiswahili sio kiarabu na bali ni kibantu
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni