KABURI LA ELIMU KWA WATOTO MASKINI
KUPANDISHA viwango vya ufaulu
bila uboreshaji wa elimu ni kuwazika watoto wa kimaskini ili waagane na
elimu ili kesho waje kuwa wapambe na watumwa wa watoto wa viongozi wa
sasa na wale wa matajiri.
Kabla hamjasimamia mipango yenu, hebu nanyi waleteni watoto wenu wasome na watoto wetu shule za umma (shule za kata).
Acha niwape kisa cha binti wa kijakazi aliyekuwa akiwania umalkia katika Taifa la Azania.
Katika Taifa la Azania alitokea mfalme ambaye maisha yake yote hadi
anafika uzee hakubahatika kupata mtoto. Mfalme alitaka akiondoka duniani
awe amempata mrithi wake ili aiche nchi salama.
Mfalme aliona awamu
inayokuja iongozwe na mwanamke aweze kuwa malkia wa Azania. Mfalme
alimwagiza msaidizi wake asimamie mchujo kisha mchujo nao ulimalizika
kwa kuwapata mabinti wawili mmoja binti wa kiongozi na mfanyabiashara
maarufu na wa pili akawa wa kijakazi, kwa hiyo lazima apatikane mmoja
aweze kuwa malkia.
Mfalme akapanga siku ya zoezi la kumpata Malkia
wa Azania na siku ilipowadia, mfalme aliwapatia zoezi dogo la kusaga
mahindi apate unga wa ugali. Mfalme aliwaletea kiroba cha mahindi kila
mmoja, akawatuma wakasage mahindi hayo wamletee unga kabla jua
halijazama.
Binti wa kiongozi na mfanyabiashara maarufu alikwenda
kwa wazazi wake na kuomba fedha za kusaga mahindi hayo kwa mashine na
kufanikiwa kusaga na kuwahi kurudi kwa mfalme.
Mtoto wa kijakazi
naye alimfuata mama yake kuomba ampatie fedha za kusaga mahindi hayo,
mama yake alimpatia jiwe. Binti wa kijakazi alisaga mahindi hayo kwa
taabu na nguvu kubwa kwa kutumia jiwe akapata unga na kuupeleka kwa
mfalme.
Baada ya kufika kwa mfalme, aliwapokea na kuwapa chekecheo
la kuchekecha unga huo kila mmoja akaanza kuchekecha. Binti wa kiongozi
na mfanyabiashara maarufu alipata unga mwingi na chenga chache, yule wa
kijakazi alipata chenga nyingi na unga mchache.
Ukweli ni kuwa binti
wa kwanza alipata unga mwingi sababu alisaga kwa mashine na binti
kijakazi alipata unga mchache kwa kuwa alitumia jiwe. Matokeo ya jumla
mfalme alimtangaza binti wa kiongozi na mfanyabiashara kuwa Malkia wa
Azania na binti wa kijakazi kwa juhudi kubwa aliambulia patupu.
Kisa
hiki cha binti wa kijakazi nakifananisha na elimu ya Tanzania na
matokeo haya ya kidato cha nne yanayoonesha watoto wetu wamefeli kwa
takriban asilimia 70. Tujiulize tunawapeleka wapi hawa? .
Ushindani
wowote ule unahitaji maandalizi ili uweze kushinda na ukiona baba au
kocha wako anakupeleka kwenye mashindano makubwa yasiyoendana na
maandalizi mazuri, ujue amepanga kukudhalilisha kama siyo kukudhalilisha
ni kukuua kabisa.
Tujiulize kushindwa kwa binti kijakazi ni uzembe
wake? Ujinga wa mama yake? au umaskini wao? Ila kwangu mimi kushindwa
kwa binti wa kijakazi ni ujinga wa mfalme kutofikiria njia gani atumie
ili zoezi litendeke kwa usawa.
Tuachane na hayo ya binti wa kijakazi na umalkia wa Azania, turudi hapa kwetu tuitazame elimu yetu ilipo na inapoelekea.
Serikali ya Awamu ya Tano imekuja na Waziri mpya Prof. Joyce Ndalichako.
Kama kawaida yetu, Watanzania tunawapima watendaji kwa majina na siyo
mafanikio ya utendaji wao. Alipoingia tu akaanza kugombania suala la
"Division" na "GPA" badala ya kuja na mpango mkakati wa kupandisha
kiwango cha elimu kiweze kupanda juu na akashinda vita hiyo ya kurudisha
"division" na kutupilia mbali "GPA" kwa kutumia mamlaka aliyonayo
badala ya uhalisia.
Elimu ya nchi yetu imeshuka sana tena kwa kiwango cha juu, kuipandisha inahitaji muda.
Elimu bora inakuwepo pindi mambo yafuatayo yanapotekelezwa;
Mosi, Kuandaliwa Sera nzuri ya elimu inayotekelezeka.
Pili, Uandaaji mzuri wa walimu
Tatu, Kuwepo kwa zana za kujifunzia na ufundishaji kama vile vitabu vya kiada na ziada.
Nne, Mandhari nzuri ya kusomea na ufundishaji.
Hoja yangu ni juu ya upandishaji viwango vya ufaulu. Tumesikia Waziri
wa Elimu Prof. Ndalichako ameturudisha katika mfumo wa madaraja, tafsiri
nyepesi ni kuwa amepandisha viwango vya ufaulu.
Mtanishangaa sana kupinga kuwapima watoto wetu katika viwango vya juu, sababu ninazo na nitasimamia hata niwekewe kisu.
Viwango vya upimaji hupandishwa endapo elimu itazidi kuboreka. Dunia
nzima inajua kuwa elimu yetu ipo chini. Wakati ni sasa tumwambie Mama
Ndalichako aboreshe kwanza elimu iwe bora ndiyo apandishe viwango vya
ufaulu.
Kuwapima watoto wa shule za S.t Kayumba na hao wenu
wanaosoma shule za academia ni dhuluma ya wazi na matabaka haya
mnayoyatengeneza majibu yake mtakuja kuyaona huko mbeleni.
Kisa cha
binti wa kijakazi hakina tofauti na uamuzi wa Prof. Ndalichako wa
kupandisha viwango vya ufaulu wa mitihani bila ya kuwa na maandalizi
yeyote aliyoyafanya kuwasaidia watoto wa kimaskini.
Ndalichako wewe
ni mtafiti mzuri tu, alichokifanya Prof. Mchome aliona kuwa elimu
imeshuka kwa sababu ina upungufu mkubwa. Hivyo basi, ili watoto wa
maskini wa Tanzania wasionewe na mfumo, aliamua kushusha viwango vya
ufaulu ila siyo kwa kutangaza wazi ili watoto wa maskini hao wasionewe
na mfumo.
Wazazi wa watoto maskini mnaosemesha watoto wenu shule za
umma na ambao mlifurahia kuisikia kauli ya Ndalichako kurudisha
madaraja, mfahamu wazi mlifurahia tanzia za elimu za watoto wenu na
kuhalalisha kusonga mbele kwa watoto wao wanopata elimu bora ili kesho
waje kuwa viongozi na kuwashinda watoto wenu kwenye soko la ajira.
Kuwapima sawa watoto wa shule za umma na wa shule binafsi ni kutaka
kuwaita watoto wetu majina mabaya kuwa hawana akili, vilaza, wazembe,
hawapendi elimu, hawana future na kashfa kibao, huku mnajua walimu wao
hamuwalipi vizuri, wanawadai madeni yasiyolipika, walimu wao
hawaandaliwi vizuri.
Wakati huohuo hamjawaletea zana za kujifunzia,
mazingira yao kujifunzia hayaridhishi pia mmewatupia na jinamizi la
lugha ya kufundishishia (Kiingereza) tusitegemee watafanya vizuri hawa.
Rai yangu kwa waziri husika boresha elimu kwanza kabla ya kupandisha
viwango vya ufaulu. Namshauri pia afikirie upya upimaji wa wanafunzi ili
kuleta usawa kutokana na elimu inayotolewa ili tupunguze mwanya uliopo
sasa.
Inabidi mtafute suluhu juu ya lugha ya kufundishia na mfumo wa
sasa ufumuliwe ili tujikite zaidi kwenye kutoa maarifa na siyo
kuwakaririsha.
Hawa watoto robo tatu waliopata daraja la nne na
sifuri tuwaweke katika uangalizi maalum, watafutiwe namna ya wao pia
kuvuka hiki kizingiti. Ni wazi uwezo wao ni mzuri ila mazingira
hayakuwaruhusu wapenye kwenye chujio lenu.
Pia mmemtaja shujaa wa
shuleni zenu tunawaomba nasi mtutajie shujaa wa shule zetu za umma hata
huyo wa kwenu akiitwa Ikulu na wa kwetu pia aitwe Ikulu kapambana kwa
juhudi zake kuliko huyo wa kwenu aliyesoma kama mfalme.
Mwisho
wabunge mfikirie kuweka sheria kwa viongozi wa serikali, wabunge na
watumishi wa umma kusomesha watoto katika shule za umma labda ndiyo
wataboresha elimu yetu, bila hivyo kilio hiki hakitaisha.
Taifa lenye madaraja tofauti ya elimu ni bomu linalongoja kulipuka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni