Baadhi ya viongozi wa dini na wananchi wamesema shutuma za aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.
Willibrod Slaa kuwa baadhi yao walihongwa na Mgombea Urais wa Ukawa
kupitia Chadema, Edward Lowassa, ni upuuzi mtupu.
Wamemtaka atoe ushahidi wa madai hayo kwa kutaja majina ya viongozi na
kiasi walichohongwa, wakisisitiza kuwa hizo ni siasa za majitaka na
kwamba anaifanyia kazi CCM ili apate njia ya kurudi katika chama hicho.
Rais wa TEC azungumza
Akizungumzia shutuma hizo, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa
Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severin Niwemugizi, amemtaka Dk.
Slaa kutoa ushahidi wa madai yake kuwa maaskofu wa kanisa hilo
wamehongwa na Edward Lowassa.
“Hizo taarifa ndiyo nazisikia kwako, lakini kama kweli amesema hivyo kwa
nini hakuweka ushahidi kuanzia majina ya maaskofu hao waliopewa fedha,
kiasi na zilikopokelewa. Lakini kwa upande wangu binafsi sijapokea kiasi
chochote kutoka kwa mtu yeyote." Amsema askofu huyo
Askofu Niwemugizi alimtaka Dk. Slaa kutoa uthibitisho wa maaskofu wa
kanisa hilo kupokea fedha kutoka kwa Lowassa waweze kutoa uamuzi.
“Lowassa nimewahi kukutana naye nilimwalika kwenye shule yangu ya
seminari kule Biharamulo… shule yenyewe inaitwa Katoke na nilimuweka
wazi sababu za kumwalika na sikupokea kiasi chochote cha fedha kutoka
kwake,”alisema askofu huyo na kuongeza:
“Athibitishe hilo aonyeshe kiasi cha fedha na majina ya maaskofu, mimi
sijapata kiasi chochote labda kama nimetupiwa kwenye akaunti yangu bila
mimi kujua lakini nasisitiza atoe ushahidi.”
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za
Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini nchini, Askofu wa Kanisa la
Kiinjili la Kipentekosti, William Mwamalanga alisema kauli za Dk. Slaa
zina dalili ya kuleta kisasi fulani.
“Angekuja mapema kabla ya taratibu hizi kuanza tungemwelewa lakini kwa
sasa yupo nyuma ya wakati. Kwanza ameonekana amesukumwa afanye
aliyofanya na hilo haliwezi kuwabadilisha Watanzania walioamua kutaka
mabadiliko,”alisema na kuongeza:
“Hotuba yake haina mashiko na taifa halihitaji watu wabinafsi,”alisema Mchungaji Mwamalanga.
Askofu Gwajima azungumza
Naye Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amekana kuwa
mshenga wa Edward Lowassa kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendelea
(Chadema) .
Pia amekana kuhusika kuwarubuni kwa fedha maaskofu 30 wa Kanisa Katoliki
ambao wanadaiwa kumuunga mkono Lowassa katika mbio zake za urais baada
ya kuhongwa fedha.
Askofu Gwajima amesema Dk. Slaa ndiyo risasi ya mwisho iliyokuwa imebakia ndani kati ya bunduki ya CCM ili kuwaokoa.
Amesema yote yaliyosemwa na Dk. Slaa ni tuhuma za uongo hivyo wananchi
wazipuuze kwa kuwa mwanasiasa huyo anatafuta uungwaji mkono kwa wananchi
aelekee CCM.
“Yaani ni uongo kabisa tena uongo mweupe, imedhihirisha wazi kuwa huyu
mtu asingefaa kuwa rais. Ni dhahiri ameona akiwasema wanasiasa wenzake
watamjibu kwenye majukwaa yao ya siasa, lakini sasa amewasema maaskofu
kwa kuwa wao hawana majukwaa.
“Kwa hiyo namshauri hayo mambo ya kuwahusisha maaskofu na uchaguzi aache
uongo wa namna hiyo. Nafikiri awaseme wanasiasa wenzake kuzungumzia
mambo ya siasa ila kuwahusisha maaskofu si mambo ya busara,” alisema.
Akizungumzia suala la kuwa mshenga wa Lowassa na Chadema, Askofu huyo
amesema anafikiri Dk. Slaa ametumwa na waliomtuma, hivyo anawafanyia
kazi watu.
“Kwa kawaida inashangaza kwamba kama watu wawili wanagombana, inatakiwa
awepo mtu wa kuwaunganisha, ila anaposema maaskofu 34 haileti maana,
haiingii akilini… ameingiza Gwajima, Rostam (Aziz) na maaskofu,
haeleweki anachozungumza. Lakini ninachosema kuna waliomtuma ni watu
ambao anawafanyia kazi.
“Kikubwa ni kwamba baada ya Lowasaa kuchaguliwa kugombea urais kwa
Chadema alichukia, alifikiri Lowassa hataendelea kuwa na umaarufu, sasa
anaona Lowassa anakwenda, hiyo imemtia hasira anataka kumchafulia
Lowassa, ndiyo maana anaongelea Lowassa Lowassa tu.
“Kwa mfano alisema Lowasa angekuja na wabunge wenyeviti wa CCM, ina
maana angemkubali Lowassa aje nao, sasa angekuja nao asingekuwa fisadi?
Ni swali zuri ila amekwepa kulijibu.
“Nafikiri Dk. Slaa ndiyo risasi ya mwisho iliyobakia ndani ya bunduki ya
CCM. Natoa wito kwa waumini wangu wafahamu kuwa hizi tuhuma ni za uongo
na namsihi huyo daktari asihusishe maaskofu na uongo wake abaki nao
mwenyewe,” alisema Askofu Gwajima.
BOFYA HAPA CHINI KUONA VIDEO YA LOWASSA NA MAGUFULI WAKIWA KWA WAGANGA WAO KUTAFUTA USHINDI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni