SAA 10.00 jioni ile ya Aprili 12, 1984, Redio Tanzania Dar es Salaam
(RTD), sasa Redio ya Taifa ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)
ilikatiza ghafla matangazo yake ya kawaida, kisha ukapigwa wimbo wa
taifa wa “Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania…”
Baada ya wimbo huo kumalizika huku wasikilizaji waliokuwa karibu na
redio iwe nyumbani, ofisini na sehemu nyingine wakishangaa na kutaka
kujua kwamba kuna nini, wote walipigwa bumbuwazi zaidi waliposikia sauti
nzito, sauti ya huzuni na isiyokuwa katika ubora na madoido yake
walivyoizoea ikieleza:
“Ndugu wananchi, leo saa saba mchana, ndugu yetu na kijana wetu, Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Edward Moringe Sokoine
alipokuwa akisafiri kutoka Dodoma kuja Dar es Salaam, gari yake ilipata
ajali. Amefariki dunia!”
Ilikuwa hotuba fupi kuliko zote zilizowahi kutolewa na Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tangu akiwa Rais wa Chama cha
Tanganyika African National Union (TANU), Waziri Mkuu wa Serikali ya
Madaraka ya Ndani (ya Tanganyika), Waziri Mkuu wa Tanganyika huru, Rais
wa Tanganyika, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hata vinginevyo.
Ilikuwa ni fupi kuliko zote ikiwa ni ya kwanza na ya mwisho kwake kwa
taifa na hata kimataifa, hotuba ambayo hadi leo imebaki ni rekodi katika
maisha yake yote akiwa ni kiongozi wa kitaifa na kimataifa.
Hotuba hiyo ilileta jitimai na simanzi kubwa nchini ambapo kwa mfano,
akina mama waliokuwa wakiuza maandazi na vitumbua katika eneo la Mtoni
Kwa Azizi, Temeke jijini Dar es Salaam ‘walichanganyikiwa’, wengi
wakajikuta wakisahau biashara zao na kuanza kukimbia ovyo mitaani huku
wakiangua vilio vya kufiwa na mpendwa wao.
Kana kwamba haitoshi, kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya Taifa ya Umoja
wa Wanawake Tanzania (UWT) kilichokuwa kikifanyika Ofisi Ndogo ya Makao
Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, kilisambaratika bila
kuahirishwa baada ya Mwenyekiti wake ambaye sasa ni hayati, Sofia Kawawa
kuwatangazia wajumbe kuhusu msiba huo mzito na wa ghafla mno.
Kina mama hao wote, kila mmoja utadhani wameamrishwa waliangua kilio
kama mtoto aliyekutana na paka mwenye vichwa saba usiku wa manane, kisha
wakaondoka na kuachana kama wanyama bila ya kuagana.
Aidha, mwanaume mmoja aliyekuwa akisubiri usafiri wa daladala katika
Kituo cha Posta ya Zamani, katikati ya jiji hilo la Dar es Salaam naye
alisikika akisema: “Ni bora hata angekufa baba yangu mzazi kuliko kufa
kwa Sokoine!”
Edward Moringe Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tatu wa nchi hii
alizaliwa Agosti Mosi, 1938 huko Monduli Juu, wilaya ya Monduli mkoani
Arusha katika familia ya kifugaji.
Aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara
yake ya kwanza Februari 13, 1977 na kutumikia nafasi hiyo hadi Novemba
7, 1980 alipojiuzulu na kwenda kusoma Chuo Kikuu cha Sofia, Bulgaria.
Aliporejea nchini miaka miwili baadaye aliteuliwa tena kushika wadhifa
huo Februari 24, 1983 na kuendelea nao hadi alipokufa kwa ajali Aprili
12, 1984 katika eneo la Dakawa (ambalo sasa lipo wilaya ya Mvomero)
mkoani Morogoro.
Kifo chake hicho ambacho kilitokea alipokuwa akisafiri kutoka katika
kikao cha bunge mjini Dodoma, kilisababishwa na benzi alilokuwa
akisafiria kugongwa uso kwa uso na gari aina ya Toyota Land Cruiser
iliyokuwa ikiendeshwa na mpigania uhuru wa chama cha African National
Congress (ANC) cha Afrika Kusini, Dumisan Dube.
Wakati alipokufa, Sokoine tayari alikuwa amejitengenezea taswira ya
uzalendo mkubwa kabisa kwa nchi yake, yule ambaye hadi leo inaaminika
kuwa ukimwondoa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hakuna kiongozi
mwingine yeyote wa kisiasa au wa umma aliyefikia uchapakazi wake,
uadilifu wake, utendaji wake na hata vinginevyo.
Katika hotuba yake ya mwisho kwa taifa alipokuwa akiahirisha kikao cha
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma hapo Aprili 11,
1984 alisema:
“Ni kheri mkulima atakayekamatwa akiiba mbolea ili (aende) akaitumie
vizuri shambani kwake, huyo (tukidhibitisha hivyo) tutamsamehe, lakini
ole wake kiongozi atakayekamatwa kwa (tuhuma za) kufanya ubaridhifu wa
mali ya umma”.
Kauli hiyo thabiti katika hali zote ilikuwa ikitoka kinywani mwa mtu na
kiongozi aliyekuwa akichukia sana rushwa, ubinafsi na wizi wa fedha za
serikali.
Ilitoka mdomoni mwa Waziri Mkuu aliyekuwa akisimamia kauli zake, yule
ambaye kile anachosema ndicho alichokuwa nacho moyoni na siyo kwa
kuigiza kama wanavyofanya viongozi wengi serikalini, vyama vya siasa na
sehemu nyingine za utawala na uongozi wa umma.
Aliishi maisha ya kawaida tofauti na wadhifa wake huo wa juu kabisa
ukiwa ni wa tatu baada ya Rais, wakati huo akiwa ni Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na Makamu wa Rais, kipindi ambacho alikuwa Ali Hassan
Mwinyi ambaye sasa ni Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili.
Alikuwa hajikwezi wala kuishi tofauti na maisha wanayoishi wananchi
walio wengi, hivyo ukiondoa tu itifaki za kiserikali alizokuwa ni lazima
apewe hakuwahi kabisa kuishi kifahari kama wanavyoishi viongozi wa leo.
Ukiachilia mbali ‘utajiri’ wa ng’ombe alioachiwa urithi na wazazi wake
kule Monduli, Sokoine kamwe hakuwahi kumiliki mali nyingine yoyote
yakiwemo mavazi ya gharama.
Maisha yake hayo yaliwekwa hadharani na Rais Julius Nyerere wakati wa
mazishi ya Waziri Mkuu huyo wa zamani huko Monduli aliposema:
“Edward Sokoine hakuwa na mali yoyote. Ukiacha ng’ombe alioachiwa urithi
na wazazi wake alikuwa na mashati matatu, suruali tatu na viatu pea
mbili!”
Nani kama yeye?
Bila hata kuwazungumzia mawaziri, naibu mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu
wa wilaya ama wabunge kamwe hakuna hata diwani, afisa mtendaji wa kata,
mtaa au wa kijiji, mwalimu wa shule ya msingi wala karani tu wa masjala
mwenye mashati matatu, suruali tatu na viatu pea mbili tu kama
ilivyokuwa kwa Sokoine!
Leo viongozi wetu au watumishi wa serikali wanashindana kwa mavazi, tena ya gharama wakionyeshana nani anayevaa kuliko mwingine.
Wanatambiana kuwa nani anayevaa nadhifu kwa mashati, suruali, suti,
viatu, saa au magauni, sketi, blausi na kusuka nywele za gharama kubwa
zaidi kushinda wenzake na hata vinginevyo.
Yule anayebadilisha mashati yake matatu, suruali zake tatu, viatu pea
mbili, magauni matatu, sketi tatu au blausi tatu huku akisuka nywele za
kawaida au kunyoa siku zote anaonekana mshamba na mtu aliyepitwa na
wakati!
Maisha yake hayo ya haki ndiyo yaliyompa jeuri ya kukemea aina zote za
hujuma, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma kama alivyosema katika hotuba
yake ile ya mwisho kwa taifa, Dodoma Aprili 11, 1984:
“Ole wao viongozi wanaotumia nafasi za madaraka yao ya umma (kwa ajili
ya) kuiba, kuhujumu uchumi au kupokea rushwa maana salama yao ni
majaliwa ya Mwenyezi Mungu na labda nisiwajue”.
Mbali na maneno hayo mazito, Waziri Mkuu huyo wa zamani ambaye kifo
chake kiliacha kila aina ya simanzi, majonzi na kumbubujisha machozi
hadi Mwalimu Julius Nyerere alipouona mwili wake, Ikulu baada ya
kufikishwa hapo kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam pia
alisema, jana yake kule bungeni:
“Nasikia kuna viongozi wa umma huko mikoani wanagombania magari badala
ya kugombania maendeleo ya wananchi, naagiza tabia hii ikome mara moja”.
Hayati Edward Sokoine anakumbukwa pia kwa kusimamia vita dhidi ya
wahujumu uchumi kuanzia mwaka 1983 – 1984 alipokufa kwa ajali, ile
ambayo hata hivyo “aliondoka nayo kaburini”.
Katika hotuba yake kwa Watanzania wakati wa mazishi ya kiongozi huyo
yaliyofanyika nyumbani kwake kule Monduli Juu, Arusha, Baba wa Taifa,
wakati huo akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa siri
nyingine ambayo ni vigumu kukubalika.
Alisema kwamba kabla ya kifo chake hicho, Sokoine alilalamikia ukubwa wa
baraza la mawaziri, hivyo akashauri lipunguzwe na kuwa dogo kulingana
na mahitaji na uwezo wa taifa kiuchumi.
Ingawa ushauri huo ungeweza pia kutolewa na mtu mwingine yeyote,
kilichomshangaza hata Mwalimu Nyerere ni kauli ya Sokoine kwamba
likivunjwa na kuundwa upya, yeye mwenyewe alikuwa radhi na tayari
kutoteuliwa tena kama rais huyo wa kwanza wa nchi hii angeona hamhitaji
tena!
Sokoine aliyekufa kwa ajali akiwa na umri wa miaka 45, miezi minane na
siku 12 kamili alianza elimu yake ya msingi mwaka 1948, kulekule
Monduli, wakati huo ikiitwa wilaya ya Masailand alikosoma hadi darasa la
nane.
Kutoka huko aliendelea na masomo katika Shule ya Sekondari Umbwe, Moshi
mkoani Kilimanjaro alikohitimu darasa la 10 mwaka 1958 na kujiunga rasmi
na chama cha TANU mwaka 1961.
Kuanzia mwaka 1962 – 1963 alisomea uongozi na utawala katika iliyokuwa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani Mashariki. Aliporejea nchini,
wakati huo akiwa kijana mwenye umri wa miaka 25 aliajiriwa serikalini
akiwa Afisa Mtendaji wa Wilaya ya Masailand.
Miaka miwili baadaye aligombea na kuchaguliwa kuwa mbunge wa wilaya hiyo
ambayo sasa iliitwa Monduli, fursa iliyompa mwanya wa kuonyesha zaidi
kipaji chake kikubwa katika uongozi na utumishi wa umma.
Ilikuwa kipindi hicho ndipo alipoteuliwa kuwa Waziri Mdogo wa Kazi,
Mawasiliano na Uchukuzi mwaka 1967, kisha akateuliwa kuwa Waziri wa Nchi
Katika Ofisi ya Rais (Usalama) ilipofika mwaka 1970.
Miaka miwili baadaye hapo mwaka 1972, Sokoine aliteuliwa na Rais Julius
Nyerere kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa hadi Februari
13, 1977 alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na kubadilishana nafasi na mtangulizi wake, Rashid Mfaume
Kawawa.
Akiwa amechaguliwa kwa mara yake ya tatu mfululizo kuwa Mbunge wa
Monduli mwaka 1975, Sokoine aliingia kwa mara ya kwanza pia katika
ujumbe wa Kamati Kuu ya TANU, kisha akawa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM
mpaka Novemba 7, 1980 alipojiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu kwa matakwa
yake mwenyewe.
Alirejea katika chombo hicho cha juu kabisa kisiasa alipoteuliwa tena
kuwa Waziri Mkuu wa nchi hii ilipofika Februari 24, 1983 hadi Aprili 12,
1984 alipopata ajali ile barabarani, eneo la Dakawa, Morogoro na kufa
papo hapo.
Katika kutambua mchango wake mkubwa kwa taifa, serikali ilikigeuza
kilichokuwa Kitivo cha Kilimo cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kampasi
ya Morogoro na kuwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, maarufu kwa
kifupi cha SUA.
Historia inaonyesha kwamba kilianzishwa mwaka 1964 kama Chuo cha Kilimo
kilichokuwa kinafundisha na kutoa stashahada (au diploma) za kilimo,
kisha kikapandishwa hadhi na kuwa Kitivo cha Kilimo cha Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam hapo mwaka 1969.
Akiwa ni kiongozi mwandamizi wa taifa, Sokoine anakumbukwa hadi leo,
miaka 32 baada ya kifo chake siyo kwa sababu alikuwa Waziri Mkuu kwani
wadhifa huo umeshashikwa pia na wanasiasa wengine akiwemo mrithi wake
alipofuka mwaka 1984, Balozi Dk. Salim Ahmed Salim.
Wengine waliowahi kushika wadhifa huo ukimwondoa Mwalimu Julius Nyerere,
Kawawa na Waziri Mkuu wa sasa, Majaliwa Kassim Majaliwa ni Cleopa David
Msuya, Joseph Sinde Warioba, John Samwel Malecela, Frederick Tluway
Sumaye, Edward Ngoyai Lowassa pamoja na Mizengo Kayanza Pinda.
Hayati Sokoine anakumbukwa hadi leo kwa sababu aliamini, kusimama na
kupigana kwa vitendo ili kutetea haki kwa wote, usawa usiokuwa na
ubaguzi pamoja na uwajibikaji kazini katika utumishi wa umma.
Alikuwa ni mzalendo wa kweli aliyeishi na kuamini katika misingi halisi
ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, kiongozi ambaye wakati wake wote
alikuwa mchapakazi na mtu asiyejua kujikweza.
Ndiyo maana alifanya kazi mpaka usiku wa manane na hata alipokuwa
barabarani akipitia mafaili na nyaraka mbalimbali, akatoa maelekezo ya
kufanya kwa wasaidizi wake kuanzia ofisini hadi mawaziri, wakuu wa mikoa
na watendaji wengine serikalini.
Alikuwa akichukia na kupambana kwa nguvu zake zote dhidi ya vitendo
vyote vinavyohusu ubadhirifu wa fedha na mali za umma, wizi wa aina
zote, kutowajibika au uzembe kazini hususan katika utumishi wa umma,
rushwa, uhujumu uchumi, ulanguzi pamoja na magendo.
Aliamini kuwa “Siasa ni Kilimo” na ndiyo maana siku zote aliipigania
sekta hiyo kwa kauli na vitendo. Alitaka Tanzania ijitosheleze yenyewe
kwa chakula, iiuze nje ya nchi ziada na kuzalisha kwa wingi mazao yote
ya biashara kama ya pamba, kahawa, chai, mkonge, kakao na kadhalika ili
kuliingizia taifa fedha za kigeni.
Alifanya hivyo akiamini pia kuwa kilimo ni uti wa mgongo. Hakutaka taifa
liwe ombaomba ila lenye nguvu kiuchumi. Ndiyo maana alijitahidi
kuliwekea msingi imara wa maendeleo kupitia elimu ya kujitegemea na siyo
ya kutafutia kuajiriwa.
Ndiyo maana hadi leo, Jumanne Aprili 12, 2016 ikiwa ni miaka 32 kamili
baada ya kifo chake kilichotokea kwa ajali ya barabarani Aprili 12,
1984, Watanzania bado wanazidi kumlilia utadhani amekufa jana na
kushindikana kabisa kumsahau.
Mungu aendelee kuiweka roho yake mahali pema peponi. AMEN
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni