WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Rais Dk. John Pombe
Magufuli kutengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Bw. Charles
Kitwanga umefuata kanuni za utumishi wa umma ambao unakataza mtumishi
kulewa akiwa kazini.
“Zipo sheria za utumishi ambazo mtumishi hatakiwi kunywa pombe na wala
hapaswi kulewa akiwa kazini… mtumishi anapaswa kuwa na akili timamu
inayokuwezesha kufanya kazi za Serikali,” alisema.
Ametoa ufafanuzi leo usiku (Ijumaa, Mei 20, 2016) wakati akijibu swali
la mwandishi wa TBC1 aliyetaka kujua kama taarifa zilizoenea kuhusu
kutenguliwa kwa Waziri huyo ni za kweli.
“Ni kweli Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Charles Kitwanga kuanzia leo tarehe
20 Mei, 2016 baada ya kuonekana amelewa wakati wa kazi. Na hili
lilibainika pale alipokuwa akijibu maswali ya wizara yake leo asubuhi,”
alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amesema kuna swali aliloulizwa ambalo hakulijibu vizuri na
kwamba swali hilo litapaswa kurudiwa kuulizwa baada ya wabunge kuomba
muongozo wa swali hilo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA, MEI 20, 2016
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni