• Breaking News

    NEVER SAY NEVER

    chief kamchicha

    chief kamchicha

    Jumanne, 8 Machi 2016

    SEFUE ALIVYONG'OKA IKULU.


    ALIYEKUWA Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ameelezea sababu zilimfanya Rais Dk. John Magufuli kumwondoa katika wadhifa huo.


    Siri za kiongozi huyo kuondolewa zimeendelea kufichuka, huku mwenyewe akisema zama za mabadiliko chini ya uongozi wa Rais Magufuli ndizo zilizomwondoa Ikulu.


    Rais Magufuli alitangaza kumn’goa Balozi Sefue juzi na kueleza kuwa atampangia kazi nyingine, huku akimtangaza Balozi Mhandisi John Kijazi kushika wadhifa huo.


    Balozi Kijazi Ikulu ya Dar es Salaam katika tukio ambalo lilichukua takribani nusu saa likihudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na baadhi ya makatibu wakuu.


    Akizungumza na waandishi wa habari baada ya shughuli hiyo, Balozi Sefue alijibu maswali mawili tu huku akimtakia heri mrithi wake huyo.


    Alisema anamshukuru Rais Magufuli kwa kumwamini katika kipindi alichoingia madarakani, lakini zimekuja zama za mabadiliko.


    “Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kushika nafasi hii. Namshukuru Rais Magufuli aliyeniamini na kuendelea kufanya kazi na mimi… Awamu hii inawasilisha mabadiliko makubwa ndiyo maana naondoka…Namtakia mwenzangu kila la heri katika kazi zake,” alisema.


    Hata hivyo wakati Balozi Sefue akijibu swali la  pili aliloulizwa na mmoja wa waandishi wa habari kuhusu uzoefu wake kwa Rais Magufuli alipojibu ‘Hapa Kazi Tu’ ghafla walikuja maofisa wa usalama kumchukua na kisha kumsindikiza moja kwa moja hadi katika gari lake.


    Katika tukio hilo la kumwapisha Balozi Kijazi, Rais Magufuli hakuwa amechangamka kama ambavyo amekuwa akionekana katika matukio mengine yanayofanana na hayo.


    Rais Magufuli ambaye aliingia saa 4:15 ukumbuni na kisha kupigiwa wimbo wa Taifa na bendi ya polisi na baada ya hapo alimwapisha Balozi Kijazi akisaidiwa na Balozi Sefue mwenyewe ambaye alimpa kitabu cha kiapo na nyaraka za ofisi.


    Tofauti na Magufuli, Balozi Sefue alionekana mchangamfu na hata kabla ya shughuli hiyo kuanza alikuwa akizungumza na Balozi Kijazi wakiwa wamesimama ndani ya ukumbi huo.


    Wakati Sefue akieleza mabadiliko kama msingi wa yeye kuondolewa, habari ambazo gazeti hili limezipata toka Ikulu zinadai kuwa kuondolewa kwake kwa namna moja au nyingine kumechangiwa na uteuzi uliozua utata wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk. Carina Wangwe.


    Inadaiwa Balozi Sefue kwa nafasi yake, alitoa baraka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama kuutangazia umma juu ya uteuzi huo, lakini baada ya muda mfupi akatangaza kuutengua.


    Waziri Mhagama  alimtangaza Dk. Carina  mbele ya kikao cha menejimenti ya NSSF akiwa na naibu wake, Anthony Mavunde.


    Dk. Carina alipaswa kuchukua nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Mkuu wa shirika hilo, Dk. Ramadhan Dau ambaye aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa balozi hivi karibuni.


    Lakini baada ya saa tano kupita, Waziri Mhagama alitoa taarifa kwa vyombo vya habari, akisema teuzi huo umetenguliwa kwa kile alichodai baadhi ya taratibu zilikuwa hazijakamilika.


    Kauli ya Waziri Mhagama, iliungwa mkono  na Balozi Sefue ambaye alisisitiza kuwa uteuzi wa Dk. Carina ulikosewa na kwamba aliteuliwa kama mwangalizi tu na si kwa kushika nafasi hiyo nyeti ndani ya shirika hilo kubwa.


    Baada ya uteuzi huo kutenguliwa yaliibuka mambo makubwa matatu yaliyotajwa kuwa nyuma ya uamuzi huo mgumu ambayo ni ukiukwaji wa sheria, utata wa uraia wake na uteuzi huo kufanywa na waziri badala ya Rais.


    Hata hivyo ni jambo moja tu ndilo lililokanushwa ambalo ni utata wa uraia wa Dk. Wangwe ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), ilitoa ufafanuzi ikisisitiza kuwa Dk. Carina ni Mtanzania halisi kwa kuandikishwa tangu mwaka 1999.


    Taarifa ya SSRA ilisema, Dk. Carina aliandikishwa kuwa raia wa Tanzania baada ya kukidhi vigezo vya kusailiwa (naturalisation)kwa mujibu wa kifungu cha 11 cha Sheria ya Uraia Na.6 ya mwaka 1995.


    Taarifa hiyo, ilieleza Dk. Carina aliukana uraia wa Uganda, ikiwa ni pamoja na kurudisha hati ya kusafiria ya nchi hiyo aliyokuwa akimiliki.


    Balozi Sefue aliyezaliwa Agosti 26, 1954 aliteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa Katibu Mkuu Kiongozi Desemba 31, 2011 akimrithi Philemon Luhanjo. Kabla ya hapo alikuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa New York, Marekani.


    Hata hivyo Desemba 30 mwaka jana Rais Magufuli alimteua tena Balozi Sefue na kumwapisha katika nafasi hiyo aliyodumu nayo kwa siku 65 tu.


    Balozi Kijazi aahidi kuendeleza utumbuaji majipu
    Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi mpya, Balozi Mhandisi John Kijazi alisema lengo la kutumbua majipu ni kuisafisha Serikali na atamsaidia Rais Magufuli kwa kazi hiyo.


    “Kuniteua maana yake ni kwamba amenipa heshima ameniamini. Haya yanayoendelea ya msamiati wa ‘kutumbua majipu’ maana yake ni kuleta nidhamu ya utendaji wa Serikali. Ni ujumbe mkubwa huu kwamba pale ambapo pana kasoro turekebishe na ndilo jukumu langu ambalo nitamsaidia Rais…” alisema Balozi Kijazi.


    Akizungumzia majukumu yake kama Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Kijazi alisema atarejesha heshima ya utumishi wa umma.


    “Kwanza kabisa mimi ndiye mkuu wa utumishi serikalini na ndiyo Katibu wa Baraza la Mawaziri na ndiye mtendaji mkuu katika ofisi ya Rais. 


     Katika kila eneo kuna majukumu ambayo inabidi tuyafanye, kwa mfano katika utendaji katika Ofisi ya Rais, mimi nitahakikisha nakuwa kiungo kikubwa kati ya Rais na wizara zake ambazo zinaunda Serikali,” alisema Balozi Kijazi na kuongeza:

    “Kama kiongozi mkuu wa utumishi Serikali napaswa kujua utumishi ukoje, mazingira ya utumishi yakoje, masuala ya nidhamu kwa watumishi yakoje, yapo ninayoyafanyia uamuzi katika ngazi yangu na yapo ambayo yatafanyiwa uamuzi katika ngazi ya juu” alisema.


    Kwa upande  wa baraza la mawaziri alisema ataendeleza jukumu la kuandaa vikao vyake na baadaye kufuatilia uamuzi uliokubaliwa.


    “Siwezi kuyafanya haya peke yangu. Kila wizara ina viongozi, ina makatibu wakuu na viongozi wengine. Itabidi niwe nafanya kazi kwa karibu na viongozi hawa ili kujua yale yanayotokea katika wizara zao na kujua yale yanayohitaji uamuzi zaidi kuliko yale wanayofanya,” alisema.


    Mbali na kusisitiza kuwafuatilia kwa karibu mawaziri katika utendaji wao, Balozi Kijazi alisema atasimamia ukusanyaji wa mapato ili kuhakikisha Serikali inakuwa na mapato ya kutosha.


    “Nadhani mmeshaona mwelekeo wa Serikali yetu, yapo mambo ya kipaumbele ambayo Rais ameshaanza kuyafanyia kazi. Suala la makusanyo ya kodi na mapato ya Serikali, kwa sababu Serikali inaendeshwa kwa mapato, wananchi watahudumiwa vizuri kama mapato yapo ya kutosha,” alisema.


    Kuhusu rushwa alisisitiza kuwa atamsaidia Rais Magufuli ili kuwa na utumishi wa umma uliotukuka.


    “Suala la kupiga vita rushwa ndani ya vyombo vyetu vya serikali, idara zetu na wizara zetu, hilo Rais ameshatoa maelekezo hivyo ni jukumu langu kuhakikisha tunakuwa na utumishi uliotukuka, wenye tija na utumishi wenye nidhamu,” alisema na kuongeza:


    “Lakini kuna utumishi wenye motisha (incentive) watumishi wanapaswa kuwa na motisha kwa majukumu waliyopangiwa,” alisema.

    Hakuna maoni:

    Chapisha Maoni

    Fashion

    Beauty

    Travel