MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHAMA ILIYOKUTANA MACHI 1, 2016, JIJINI DAR ES SALAAM
Kamati Kuu ya Chama imesema kuwa tangu utawala wa awamu ya tano chini
ya Serikali ya CCM ikiongozwa na Rais John Magufuli uingie madarakani,
misingi ya uongozi bora na demokrasia ya vyama vingi imeyumba, kiasi cha
kuiingiza nchi katika sintofahamu kubwa ya kisiasa, kiuchumi na
kiutawala na kutishia mstakabali wa nchi.
Akitoa maazimio ya
kikao cha Kamati Kuu, mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es
Salaam, Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe ametaja masuala kadhaa
ambayo yameanza kuharibu sifa Tanzania kwa kuvunja misingi ya demokrasia
kuwa ni pamoja na ‘uhuni’ wa kisiasa unaofanywa na Serikali, vyombo vya
dola kwa kushirikiana na CCM kupora haki ya wananchi katika uchaguzi wa
mameya na wenyeviti wa halmashauri hasa maeneo ambako vyama vinavyounda
UKAWA vimeshinda.
Katika muktadha huo, Mwenyekiti Mbowe amesema
kuwa Kamati Kuu katika kikao chake hicho kilichoketi Machi 1, mwaka huu,
imazimia kwa kauli moja kuwa Chadema haitaendelea tena ‘kuomba’ haki ya
kufanyika uchaguzi na hatimaye kuongoza Jiji la Dar es Salaam kupitia
Meya na Naibu wake, wanaotokana na UKAWA, bali itaidai haki hiyo, ambayo
imepatikana kutokana na mapenzi ya wananchi wa jiji hilo kwa vyama
vinavyounda UKAWA.
Mwenyekiti Mbowe amewaambia waandishi wa
habari kuwa Kamati Kuu katika kikao hicho cha siku moja, ilijadili na
kutafakari kwa kina, pamoja na masuala mengine, mambo yafuatayo:
1. Hali ya kisiasa nchini.
2. Kutathmini uhai na nguvu ya chama.
Kwa kuanzia, Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa kwa Mamlaka ya Kikatiba,
ibara ya 6.1.3 inayopewa nguvu na ibara ya 7.5.1, Chama kimeamua
kuimarisha uongozi wa kichama mkoani Dar es Salaam, kwa kuanzisha Kamati
Maalum itakayosimamia eneo linalojulikana Dar es Salaam Kuu (Greater
Dar es Salaam) ambayo pamoja na mambo mengine, wajibu wa awali itahusika
katika kuratibu upatikanaji wa haraka wa kikatiba, kisheria na kikanuni
wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti
Mbowe, Kamati hiyo Maalum itakayokuwa chini ya Uenyekiti wa Mwita
Waitara (Mb), Makamu Mwenyekiti Bernard Mwakyembe (Diwani) na Katibu
Henry Kilewo ikiwa na wajumbe 25, pia itahusika katika mambo mengine
yanayohusu uimarishaji wa chama na usimamizi wa shughuli zote zinazohusu
utendaji wa wawakilishi wa chama katika vyombo vya serikali hususan
katika eneo la Dar es Salaam Kuu.
Suala jingine
lililodhihirisha kuyumba kwa misingi ya uongozi bora na demokrasia ya
vyama vingi ni uchaguzi wa Zanzibar ambao Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa
washindi halali wa nafasi ya Rais na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
wamenyimwa haki yao hali ambayo hadi sasa imesababisha sintofahamu kubwa
ya kisiasa, kiuchumi na kiutawala Zanzibar, akisisitiza kuwa msimamo wa
Chama cha CUF ndiyo msimamo wa CHADEMA kuhusu hali tete inayoendelea
visiwani humo.
Aidha, Mwenyekiti Mbowe ameongeza masuala mengine
ambayo yameiharibia sifa nchi katika kusimamia misingi ya demokrasia na
uongozi bora, kuwa ni pamoja na namna Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
na vyombo vya dola vilivyosimamia Uchaguzi Mkuu na kutumika kupora haki
ya wananchi ya kuchagua na kupata viongozi wanaowataka.
Suala
jingine ni juhudi za makusudi zinavyofanywa na watawala wa awamu ya tano
kudhibiti mhimili wa Bunge usitekeleze wajibu wake wa kikatiba wa
kuisimamia serikali, akitolea mifano kadhaa ikiwemo kuzuia TBC kurusha
vikao vya bunge moja kwa moja, Serikali ya CCM kuingilia uundwaji wa
uongozi wa Kamati za Bunge zinazosimamia fedha za umma (PAC na LAAC).
“Pia serikali hii hii ya CCM imeingilia mhimili wa bunge na kudhibiti
uundwaji wa Kamati mbalimbali za bunge kwa kutumia visivyo au nje ya
taaluma, uzoefu na uwezo wao wabunge wa kutoka vyama vyote ambao
walionesha ujasiri wa kuikosoa Serikali katika mabunge yaliyopita…jambo
ambalo kwa upande wa Kamati za PAC na LAAC tumekataa CCM watuamulie
kinyume na sheria na kanuni za bunge.
“Jeshi la Polisi kwa
maelekezo ya Serikali limeendelea kuzuia mikutano ya hadhara na
maandamano ya vyama vya upinzani, ilihali CCM, viongozi wao, wanachama
na wafuasi wao wakifanya maandamano na mikutano maeneo mbalimbali ya
nchi bila kuzuia na polisi. Yote haya yanafanyika, Magufuli anajua,
Majaliwa anajua.
“Viongozi wetu, wanachama, wafuasi na hata
mashabiki wa vyama vya upinzani wanafunguliwa mashtaka yasiyokuwa na
msingi pale wanapodai haki za kikatiba za kutekeleza wajibu wao wa
kisiasa katika mazingira huru yenye uhakika. Wameamua hata kudhibiti kwa
kuvitisha na hata kuvifuta vyombo vya habari ambavyo vinatimiza wajibu
kikamilifu kwa jamii na havifungamani na CCM moja kwa moja. Yote haya
yanafanyika Magufuli anajua, Majaliwa anajua,” amesema Mwenyekiti Mbowe
na kuongeza;
“Ni vyema kuelewa kuwa hatua ya misingi ya utawala
bora na demokrasia ya vyama vingi ambayo kama nchi tulikuwa tumeifikia
kiasi cha Tanzania kujipambanua miongoni mwa nchi za Afrika hasa Kusini
mwa Sahara yalikuwa ni matokeo ya mapambano ya zaidi ya miaka 20
kupigania demokrasia katika taifa hili. Leo watu wanataka nchi iongozwe
kwa kauli za mtu au watu badala ya misingi ya katiba, sheria na taratibu
ambazo nchi imejiwekea.”
Mwenyekiti Mbowe amehitimisha kwa
kusema, Kamati Kuu imeazimia kwamba namna ya kukabiliana na hila, njama,
mipango ovu ya CCM dhidi ya wapinzani, hali ya kisiasa nchini kwa kina
pamoja na Mkakati wa Chama wa Miaka 5 ijayo, itajadiliwa na kufanyiwa
maamuzi katika kikao cha Baraza Kuu kitakachofanyika jijini Mwanza,
Machi 12 mwaka huu ambalo pia litaweka dira na mwelekezo wa chama
kuelekea mwaka 2020.
Imetolewa leo Machi 5, 2016 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni